KIKAO CHA CME CHATOA ELIMU YA UPIMAJI SELI MUNDU

Posted on: August 2nd, 2023


Na SRRH

ELIMU kuhusiana na huduma ya kipimo cha utambuzi wa Seli mundu (HB Electrophoresis Test) ikiwa na lengo la kuongeza uelewa na umuhimu wake kwa afya ya binadamu, imetolewa kwa watumishi leo Agosti 02, 2023 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Mtaalamu wa Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Bi. Rukia Ahmed akitoa elimu ya HB Electrophoresis Test.

Akitoa elimu hiyo katika mwendelezo wa vipindi ya Elimu ya Matibabu (CME), Mtaalamu kutoka Kitengo cha Maabara katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Rukia Ahmed, amesema kipimo hicho kinasaidia kutoa majibu ya ugonjwa wa Seli Mundu (Sickle Cell) kwa mgonjwa na upo kwa kiasi gani.

“Kipimo hiki ni muhimu kutambua hali ya ugonjwa wa Seli mundu kwa mgonjwa halikadhalika kufahamu upo kwa kiasi kipi.

“Vilevile HB Electrophoresis Test ina inaweza kumpima mtoto pindi anapozaliwa ili kugundua kama ana seli mundu na kwa kiasi gani," amesema Rukia.

Watumishi wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga wakifuatilia elimu ya HB Electrophoresis Test.

Kwa upande mwingine, Rukia ameshauri kwa watu walio kwenye mahusiano ama wanatarajia kuingia kwenye ndoa na wana ndoto za kupata mtoto ni vema wakapima ili kuweza kujua hali zao.

“Kipimo hiki kinaweza kusaidia wenza wanaotarajia kuingia kwenye ndoa kuweza kupima, maana ikigundulika wana sifa, itachangia nafasi kubwa ya wao kupata mtoto mwenye Seli mundu.

“Hivyo ni vema kupima, maana itawasaidia kujua hali zao mapema, na ukizingatia ukanda huu wa ziwa una kiasi kikubwa cha watu wenye Seli mundu”, amesema.

MAANA YA UGONJWA WA SELI MUNDU

Seli mundu ni ugonjwa wa shida ya damu unaosababishwa na hemoglobini isiyo ya kawaida iliyorithiwa (protini inayobeba oksijeni ndani ya seli nyekundu za damu). Inarithiwa wakati mtoto anapokea jeni mbili za seli mundu-moja kutoka kwa kila mzazi.