ELIMU YA LUGHA ZA ALAMA YATOLEWA KWA WATUMISHI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA

Posted on: August 10th, 2023

Na SRRH

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kupitia mwendelezo wa Vipindi vya Elimu ya Afya (CME) imetoa elimu ya mawasiliano ya Lugha ya Alama kwa watumishi kwa lengo la kusaidia kuwasiliana na wagonjwa wenye changamoto ya kutosikia (viziwi).

Akitoa elimu hiyo Agosti 09, 2023, Mkuu wa Idara ya OPD/EMD, Dkt. Kambi Buteta, alieleza kuwa elimu hiyo ni muhimu kwakuwa itasaida kutatua changamoto ya mawasiliano baina ya watoa huduma za Afya na wenye changamoto ya kutosikia.

“Elimu hii ni muhimu, mgonjwa anapofika Hospitalini kwetu kupata huduma na hawezi kuzungumza, inabidi tuwasiliane naye kwa mfumo wa lugha za alama.

“Ni vizuri tukaielewa na kuitumia sisi watumishi ili kuondoa changamoto ya mawasiliano kwa lengo la kuwasaidia wagonjwa namna hii", alisema Dkt. Kambi.

Pamoja na elimu hiyo kutolewa, Dkt. Kambi amesema elimu hiyo itaendelea kutolewa mara kwa mara kuwajengea uwezo zaidi watumishi ili waweze kuondokana na changamoto ya kutoelewana na wagonjwa wasioweza kusikia.