HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA YAADHIMISHA WIKI YA HOMA YA INI KWA KUPIMA WANANCHI 210 BURE
Posted on: July 31st, 2023
Na SRRH
KATIKA kuadhimisha siku ya Homa ya Ini Duniani iliyofanyika Julai 28, 2023, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga iliweza kupima jumla ya wananchi 210.
Kati ya wananchi 210 waliopima, 13 waligundulika kuwa na Maambukizi ya virusi vinavyosababisha Homa ya Ini (Hepatitis B) ambayo ni sawa na asilimia 6 ya waliopima, na wananchi 76 walipatiwa huduma ya chanjo ya virusi vinavyosababisha homa hiyo.
Kufuatia zoezi hilo kufanyika, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Dkt. Luzila John, amewataka wananchi kuwa na desturi ya kupima afya zao mara kwa mara, ikiwemo maambukizi ya virusi vinavyosababisha Homa ya Ini.
“Naomba kutoa Rai kwa wananchi kujenga desturi ya kupima afya zao mara kwa mara ili kuepukana na maabukizi, hususani ya virusi vinavyosababisha Homa ya Ini, vilevile kupata chanjo itakayosaidia kujikinga na madhara makubwa yanayosababishwa na virusi hivi.” amesema Dkt. Luzila.
Maadhimisho ya Homa ya Ini katika Hospitali ya Rufaa Shinyanga, yalifanyika kwa siku tatu, kuanzia Julai 26 hadi 28, 2023, ambapo Hospitali iliadhimisha kwa kutoa huduma ya Vipimo vya Homa ya Ini, pia Elimu na Ushauri bure iliyoambatana na huduma ya Chanjo.