HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA YAANZA KUTOA CHANJO YA HOMA YA INI
Posted on: July 26th, 2023Na SRRH
KUELEKEA maadhimisho ya Homa ya Ini Duniani Julai 28, 2023, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga leo Julai 26, 2023 imeanza kutoa Huduma ya Vipimo vya Homa ya Ini pamoja Chanjo (Hepatitis B) nje ya Ofisi za Hospitali zilizopo Mwawaza.
Huduma hii imeanza kufanyika huku ikiambatana na utoaji wa elimu, pamoja na ushauri nasaha kwa wapimaji ili kupata uelewa zaidi kuhusiana na Homa ya Ini.
Mwananchi akiwa tayari kupatiwa Chanjo ya Homa ya Ini na Wataalamu wa Afya katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Luzila John, ameihakikishia jamii na kuondoa hofu juu ya usalama wa chanjo hiyo, ambayo inachukua muda mfupi kutolewa, na kufafanua kuwa huduma inatolewa kwa watu wote wenye umri wa kuanzia miaka 19 na kuendelea.
“Tunawakaribisha wananchi pamoja na watumishi kuja kupata chanjo hii muhimu, tukiwa tunaelekea kwenye maadhimisho ya Homa ya Ini Duniani, ambayo hufanyika kila Julai 28 ya kila mwaka.
“Chanjo hii ni salama na nzuri, hivyo sote hatuna budi kuchanja ili kuweka afya zetu katika misingi yenye usalama zaidi”, amesema Dkt. Luzila.
Baadhi ya wananchi waliojitokeza kwa ajili ya Upimaji wa Homa ya Ini
Zoezi hili la elimu, ushauri na chanjo, litaendelea kutolewa hadi Ijumaa Julai 28, 2023 ambayo ndiyo siku rasmi ya kilele cha Maadhimisho ya Homa ya Ini ambayo kauli mbiu yake kwa mwaka huu ni “Usisubiri, Pima, Pata Matibabu, Zuia Maambukizi.