MAFUNZO YA MFUMO WA NeST YATOLEWA KWA WATAALAM SHINYANGA RS NA SRRH

Posted on: September 15th, 2023


Na SRRH

OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga kupitia Wakufunzi wake imeendesha Mafunzo ya Mfumo mpya wa Manunuzi ya Umma (NeST) kwa Wataalamu wa Shinyanga RS na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH), yaliyofanyika Septemba 12 hadi 13, 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Mafunzo hayo yamefanyika kwa lengo la kujenga uwezo kwa Wataalamu hao, ili kuwapatia uelewa wa matumizi ya kutatua changamoto ya urasimu, pamoja na ucheleweshaji katika kufanya mchakato wa manunuzi na kutoa huduma ya zabuni kwa wadau.

Wawezeshaji Gervas Lugodisha ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Ammy Mohammed ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, wote kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, katika mafunzo hayo wameeleza mfumo wa NeST ndiyo utakuwa unatumika kwenye manunuzi.

Wakufunzi wamebainisha Serikali imeanzisha mfumo mpya wa NeST kwa lengo la kufanya manunuzi yote, na haitaruhusiwa kwa Taasisi zote kufanya manunuzi kwa kutumia mfumo mwingine bila NeST sababu ni kosa kwa mujibu wa Sheria.

Ujio wa NeST imekuwa ni mbadala wa TANePS, mfumo ambao ulikuwa ukitumika awali kwa ajili ya manunuzi, ambao utafika ukomo wake rasmi ifikapo Septemba 30, 2023 na hivyo kutoa fursa kwa mfumo huu mpya wa NeST kuanza kutumika rasmi kuanzia Oktoba 1, 2023.