TAKUKURU YATOA ELIMU YA RUSHWA MAHALA PA KAZI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA

Posted on: September 20th, 2023


Na SRRH

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga, leo Septemba 20, 2023 imetoa elimu ya Rushwa mahala pa kazi kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, juu ya uzingatiaji wa maadili ya kazi yanayolenga kuepukana na Rushwa ambaye ni adui wa haki.

Akizungumza katika Ukumbi wa Mikutano wa Hospitali, Mchunguzi Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Ndg. Hosiana Uloni, amebainisha kuwa ili kuepuka kuchafua taswira ya Hospitali, ni vema utendaji kazi ukafanyika kwa ueledi bila kuomba Rushwa.

Mwezeshaji Hosiana Uloni (Mchunguzi Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga) akitoa elimu ya Rushwa kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Uloni ameeleza kuwa kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watumishi kutoa huduma kwa kuangalia muonekano wa mtu, badala ya kuzingatia haki na maadili pia miiko ambayo haileti uchochezi wa kuomba Rushwa.

“Tutoe huduma zetu kwa haki na kwa usawa, haileti picha na taswira nzuri kwa mtumishi kutoa huduma kwa kuangalia hadhi ya mtu, kuwa ni nani, anafanya kazi wapi na amevaa namna gani.

“Tujikite zaidi kutoa huduma kwa kuwajali wateja wetu tena kwa wakati, unapoomba rushwa kwa mteja wako utakuwa unachangia kuichafua taasisi yako na kupoteza ya uaminifu kwa wagonjwa ambao ndiyo wateja wenu". amesema Uloni.

Kwa upande wake Suzan Roscar ambaye ni Afisa Mchunguzi TAKUKURU mkoa wa Shinyanga, amesisitiza kwa kuwaomba watumishi kuachana na suala la kuomba Rushwa, sababu ni kosa kisheria na halikubaliki.

Mwezeshaji Suzan Roscar (Afisa Mchunguzi TAKUKURU Shinyanga) akitoa elimu ya Rushwa kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga)

Roscar ameeleza kudai ama kuomba Rushwa inachangia kwa kiasi kikubwa kuichafua Taasisi na Serikali kwa ujumla kwani ni kosa la jinai.

Aidha, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Alistid Ngalawa, ametoa pongezi kwa Ofisi ya TAKUKURU Shinyanga kwa ujio wao Hospitalini kuja kutoa elimu hiyo muhimu, huku akiwaomba watumishi kuzingatia yaliyofundishwa.

Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga wakifuatilia utolewaji wa elimu ya Rushwa kutoka kwa Wawazeshaji wa TAKUKURU

Lakini pia, Afisa Utumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, Ndg. Beatrice Gwakisa Cheyo, amewataka watumishi kuyafanyia kazi yaliyozungumziwa na akiwaomba waendelee kutoa ushirikiano na Hospitali, ikiwemo kuendelea kuja kukumbushia ili kutia hamasa zaidi ya kuondoka na mdudu Rushwa.

Mwezeshaji Hosiana Uloni akitoa elimu ya Rushwa kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.