TIMU MACHI WAKABIDHI MSAADA KWA WATOTO WACHANGA SRRH

Posted on: April 18th, 2024


Na George Mganga, SRRH

KIKUNDI cha watu waliozaliwa mwezi wa tatu (Team March) katika Manispaa ya Shinyanga, Aprili 17, 2024 kimetoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wachanga katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRR).

Akizungumza baada ya kukabidhiwa kwa vifaa, Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Sadick Kibira, alieleza lengo na dhamira ni kujali maslahi ya watoto ambao wanahitaji uangalizi mkubwa, pia kutoa motisha kwa watumishi ambao wanapambana kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto.

“Tumeamua kuunda kikundi hiki kwa ajili ya kusaidiana mambo mbalimbali yenye tija ya kuleta maendeleo,

“Kwa kuanza tumeamua kutembelea Hospitali ya Mkoa kuja kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kama sabuni, mashuka na vingine ili kuwajali watoto hawa ambao wapo kwenye uangalizi mkubwa pia kuwapa motisha wafanyakazi wanaopambania afya zao”, alisema Kibira.

Kwa upande mwingine, Kibira aliwapongeza wauguzi na madaktari katika Idara ya NICU kwa namna wanavyowajibika kutimiza majukumu yao hususani katika harakati za kuokoa maisha ya watoto wachanga.

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani, Luzila John, aliwapongeza kwa msaada walioutoa huku akiwaomba waendelee kuwa na moyo huo wa upendo kwa siku zingine.

Dkt. Luzila alieleza kuwa jambo walilofanya ni baraka kubwa kutoka kwa MUNGU, hivyo waendelee kuishi katika maisha hayo yakusaidia na kuzigusa jamii zingine kama walivyofanya kwa upande wa Hospitali.