WIZARA YA AFYA YATOA ELIMU YA UGONJWA WA SIKO SELI HOSPITALI YA RUFAA SHINYANGA

Posted on: July 26th, 2023

Na SRRH

WIZARA ya Afya leo Julai 26, 2023 imetoa elimu kuhusiana na Ugonjwa wa Siko Seli katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, kwa aili ya kuongeza wigo wa uelewa wa ugonjwa huo, hususani namna ya kujikinga na kuutibu.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani, Elisha Osati kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, amesema lengo elimu ni kuzuia ugonjwa usisambae na vilevile kutoa mwongozo wa matibabu ili kupambana na tatizo la uwepo wa Siko Seli nchini.

“Tumekuja Shinyanga kwa niaba ya Wizara ya Afya ili kuzungumzia ugonjwa wa Siko Seli, hili ni tatizo ambao ambalo lipo hapa nchini, tumedhamiria kutoa elimu ya ugonjwa huu ili kuugundua, kufanya vipimo, kuutibu.

“Tumetoa elimu hii katika Hospitali ya Rufaa Shinyanga na vilevile Hospitali zingine za jirani, lakini pia mashuleni na katika jamii mbalimbali ili kusaidia kuzuia usisambae zaidi, na hata kusaidia wenye matatizo wasiendelee kupata changamoto zaidi”, amesema Dkt. Osati.

Akiwa amembatana na Dkt. Julieth Kambengula ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa, Happiness Hadj kutoka Idara ya Tiba Wizara ya Afya, pia Marry Shadrack, Afisa Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Osaiti amebainisha kuwa Tanzania ni nchi ya tatu (3) kitakwimu Afrika na nne (4) Duniani kwa wagonjwa wenye Siko Seli, huku Mkoa wa Shinyanga ukishika namba tatu (3) Kitaifa.